Add parallel Print Page Options

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)

21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[a] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”

Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:

“Waambie watu wa Sayuni,[b]
    ‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
    Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(A)

Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:

“Msifuni[c] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
    ajaye katika jina la Bwana!’(B)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”

10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”

11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 21:2 mwanapunda wake Kifungu katika Agano la Kale ambacho Mathayo ananukuu mstari wa 5 kinasema wazi kwamba punda wa pili ni mwanapunda.
  2. 21:5 watu wa Sayuni Kwa maana ya kawaida, “binti Sayuni”, ina maana mji wa Yerusalemu. Tazama Sayuni katika Orodha ya Maneno.
  3. 21:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia mwishoni mwa mstari huu na pia katika mstari wa 15.