Add parallel Print Page Options

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mt 21:1-11; Lk 19:28-40; Yh 12:12-19)

11 Walipokaribia Yerusalemu walifika eneo la Bethfage na Bethania lililo karibu na Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, na kuwaagiza, “Mwende katika kijiji kilichopo ngambo yenu kule, na mara tu mtakapoingia ndani yake mtakuta mwana punda amefungwa mahali na ambaye hajawahi kupandwa na mtu yeyote. Mfungueni na kisha mumlete hapa. Na mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnafanya hivi?’ ninyi mseme, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha kwenu mara moja.’”

Hivyo wakaondoka, nao wakamkuta mwana punda huyo amefungwa katika mtaa wa wazi karibu na mlango. Wakamfungua. Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu na mahali pale wakawaambia, “Je, kwa nini mnamfungua mwana punda huyo?” Wanafunzi wake wakawaeleza yale walioambiwa na Yesu wayaeleze, nao wakawaacha waende zao.

Kisha wakamleta mwana punda yule kwa Yesu na wakaweka mavazi yao ya ziada juu ya mwana punda, naye akampanda na kukaa juu yake. Watu wengi wakatandika makoti yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kwenye mashamba yaliyo jirani. Wote wale waliotangulia mbele na wale waliofuata walipiga kelele kwa shangwe,

“‘Msifuni[a] Mungu!
Mungu ambariki yeye
    anayekuja katika Jina la Bwana!’(A)
10 Mungu aubariki ufalme unaokuja,
    ufalme wa Daudi baba yetu!
    Msifuni Mungu juu mbinguni!”

11 Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na kwenda hadi kwenye eneo la Hekalu akizunguka na kutazama kila kitu kilichokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, aliondoka kwenda Bethania akiwa na wanafunzi wake kumi na wawili.

Read full chapter

Footnotes

  1. 11:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia katika mstari wa 10.