Add parallel Print Page Options

Petro Atambua Yesu ni Nani

(Mk 8:27-30; Lk 9:18-21)

13 Yesu alikwenda eneo la Kaisaria Filipi na akawauliza wafuasi wake, “Watu wanasema mimi ni nani[a]?”

14 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji. Wengine wanasema wewe ni Eliya. Na wengine wanasema wewe ni Yeremia au mmoja wa manabii.”

15 Kisha Yesu akawauliza, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”

16 Simoni Petro akajibu, “Wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.”

17 Yesu akajibu, “Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona. Hakuna aliyekufundisha hilo ila Baba yangu wa mbinguni ndiye amekuonesha mimi ni nani. 18 Hivyo ninakwambia, Wewe ni Petro. Na nitalijenga kanisa langu kwenye mwamba[b] huu. Nguvu ya mauti[c] haitaweza kulishinda kanisa langu. 19 Nitawapa funguo za Ufalme wa Mungu. Mnapohukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Mnapotamka msamaha hapa duniani, msamaha huo utakuwa msamaha wa Mungu.”[d]

20 Kisha Yesu akawaonya wafuasi wake wasimwambie mtu yeyote kuwa yeye ndiye Masihi.

Read full chapter

Footnotes

  1. 16:13 mimi ni nani Kwa maana ya kawaida, “Mwana wa Adamu ni”.
  2. 16:18 Petro … mwamba “Petro”, ni jina la Kiyunani (Kigiriki) ambalo kwa Kiaramu ni “Kefa” likimaanisha “mwamba”. Katika Maandiko (Isa 51:1,2), pamoja na desturi za Kiyahudi, Ibrahimu alilinganishwa na mwamba ambao Mungu angeutumia “kujengea” watu wake. Hivyo Yesu anaweza kulinganisha kuwa Yesu ni kama Ibrahimu. Mungu aliwapa majina mapya Ibrahimu na Sara na aliwaheshimu kama mifano ya imani kwa wazaliwa wao. Katika namna hiyo hiyo, Yesu alimpa jina jingine Petro (tazama Mk 3:16) na akamheshimu hapa kwa ujasiri wake wa imani.
  3. 16:18 Nguvu ya mauti Kwa maana ya kawaida, “malango ya Kuzimu”.
  4. 16:19 Mnapotamka msamaha … msamaha wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “Kila mtakachofunga hapa duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachokifungua hapa duniani kitafunguliwa mbinguni.”