Basi sasa tutoke katika yale mafundisho ya msingi kuhusu Kristo, tupige hatua kufikia ukamilifu katika kuelewa kwetu. Hatupaswi tena kuwaeleza ninyi yale mafundisho ya msingi kuhusu kutubu na kuacha matendo yaletayo kifo, na kuhusu kumwamini Mungu pamoja na maagizo kuhusu ubatizo, kuwekea watu mikono, kufufuka kwa wafu na hukumu ya milele. Mungu akitujalia tutaendelea mbele.

Kwa maana haiwezekani tena kuwarejesha katika toba watu ambao waliwahi kuongoka, ambao wameonja uzuri wa mbinguni, wakashiriki Roho Mtakatifu, ambao wameonja wema wa neno la Mungu na nguvu za nyakati zijazo, kama wakikufuru. Kwa sababu wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu mioyoni mwao na kumwaibisha hadharani. Ardhi ambayo baada ya kupata mvua ya mara kwa mara, hutoa mazao yanayowanufaisha wale ambao wanailima na kupokea bar aka kutoka kwa Mungu. Lakini kama ardhi hiyo itaotesha magugu na miiba, haina thamani, na inakaribia kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.

Wanaopokea Ahadi Za Mungu

Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mazuri zaidi, yanayoandamana na wokovu. 10 Mungu si dhalimu hata asahau kazi yenu na upendo mliomwonyesha mlipowa saidia watu wake na mnavyoendelea kuwasaidia. 11 Tunapenda kila mmoja wenu aonyeshe bidii hiyo hiyo mpaka mwisho ili mpate kupo kea tumaini lenu. 12 Hatutaki muwe wavivu bali muige wale ambao kwa imani na subira hupokea yale yaliyoahidiwa na Mungu.

Uhakika Wa Ahadi Ya Mungu

13 Mungu alipompa Ibrahimu ahadi, aliapa kwa jina lake mwe nyewe kwa kuwa hapakuwa na mkuu kuliko yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake. 14 Alisema, “Hakika nitakubariki na kukupatia watoto wengi.” 15 Na hivyo baada ya kungoja kwa subira, Abra hamu alipata ahadi hiyo.

16 Watu huapa kwa mtu aliye mkuu kuliko wao, na kiapo hicho huthibitisha kinachosemwa na humaliza ubishi wote. 17 Kwa hiyo Mungu alipotaka kuwahakikishia warithi wa ahadi yake kuhusu maku sudi yake yasiyobadilika, aliwathibitishia kwa kiapo. 18 Mungu alifanya hivyo ili, kwa kutumia mambo haya mawili yasiyobadilika, na ambayo Mungu hawezi kusema uongo, sisi tuliokimbilia usalama kwake tutiwe moyo, tushikilie kwa uthabiti tumaini lililowekwa mbele yetu.

19 Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho zetu yenye nguvu na imara. Tumaini hili linaingia hadi ndani ya pazia 20 ambamo Yesu ameingia akitutangulia; ameingia huko kwa niaba yetu. Yeye amekuwa kuhani mkuu milele, kama Melkizedeki.

1-2 Hivyo tusiendelee tena na masomo ya msingi juu ya Kristo. Tusiendelee kurudia kule tulikoanzia. Tuliyaanza maisha yetu mapya kwa kugeuka kutoka katika uovu tuliotenda zamani na kwa kumwamini Mungu. Hapo ndipo tulipofundishwa kuhusu mabatizo,[a] kuwawekea watu mikono,[b] ufufuo wa wale waliokwisha kufa, na hukumu ya mwisho. Sasa tunahitajika kuendelea mbele hadi kwenye mafundisho ya ukomavu zaidi. Na hayo ndiyo tutayafanya Mungu akitupa kibali.

4-6 Baada ya watu kuiacha njia ya Kristo, je unaweza kuwafanya wabadilike tena katika maisha yao? Ninazungumzia wale watu ambao mwanzo walijifunza kweli, wakapokea karama za Mungu, na kushiriki katika Roho Mtakatifu. Walibarikiwa kusikia ujumbe mzuri wa Mungu na kuziona nguvu kuu za ulimwengu wake mpya. Lakini baadaye waliziacha zote, na siyo rahisi kuwafanya wabadilike tena. Ndiyo sababu wale watu wanaomwacha Kristo wanamsulibisha msalabani kwa mara nyingine, wakimwaibisha yeye mbele ya kila mtu.

Watu wengine wako kama ardhi inayopata mvua nyingi na kuzaa mazao mazuri kwa wale wanaoilima. Aina hiyo ya ardhi inazo baraka za Mungu. Lakini watu wengine wako kama ardhi ambayo huzalisha miiba na magugu tu. Haifai na iko katika hatari ya kulaaniwa na Mungu. Itateketezwa kwa moto.

Rafiki zangu, sisemi haya kwa sababu nafikiri kuwa yanawatokea ninyi. Kwa hakika tunatarajia kuwa mtafanya vizuri zaidi; kwamba mtayafanya mambo mema yatakayotokea katika wokovu wenu. 10 Mungu ni wa haki, na ataikumbuka kila kazi mliyoifanya. Atakumbuka kuwa mliuonesha upendo wenu kwake kwa kuwasaidia watu wake na kwamba mnaendelea kuwasaidia. 11 Tunamtaka kila mmoja wenu awe radhi na mwenye shauku ya kuuonyesha upendo kama huo katika maisha yenu yote. Ndipo mtakapokuwa na uhakika wa kupata kile mnachokitumaini. 12 Hatupendi muwe wavivu. Tunapenda muwe kama wale, kwa sababu ya imani yao na uvumilivu, watapokea kile Mungu alichoahidi.

13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu. Na hayuko yeyote aliye mkuu kuliko Mungu, hivyo akaweka ahadi yenye kiapo kwa jina lake mwenyewe; kiapo ambacho atatimiza alichoahidi. 14 Alisema, “Hakika nitakubariki. Nitakupa wewe wazaliwa wengi.”(A) 15 Ibrahimu akangoja kwa uvumilivu hili litimie, na baadaye akapokea kile Mungu alichoahidi.

16 Mara nyingi watu hutumia jina la mtu aliye mkuu zaidi yao ili kuweka ahadi yenye kiapo. Kiapo huthibitisha kwamba walichokisema ni kweli, na hakuna haja ya kubishana juu ya hilo. 17 Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ahadi yake ilikuwa kweli. Alitaka kuthibitisha hili kwa wale ambao wataipokea ahadi. Aliwataka waelewe kwa uwazi kwamba makusudi yake kamwe hayabadiliki. Hivyo Mungu akisema kitu fulani kingetokea, na akathibitisha aliyosema kwa kuongezea kiapo. 18 Mambo haya mawili hayawezi kubadilika: Mungu hawezi kusema uongo anaposema kitu, na hawezi kudanganya anapoweka kiapo.

Hivyo mambo yote hayo ni ya msaada mkubwa kutusaidia sisi tuliomjia Mungu kwa ajili ya usalama. Yanatuhimiza kuling'ang'ania tumaini lililo letu. 19 Tumaini hili tulilonalo ni kama nanga kwetu. Ni imara na la uhakika na hutulinda salama. Huenda hadi nyuma ya pazia[c] katika mahali patakatifu zaidi kwenye hekalu la kimbingu la Mungu. 20 Tayari Yesu amekwisha kuingia hapo na kuifungua njia kwa ajili yetu. Amefanyika kuhani mkuu milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.

Footnotes

  1. 6:1-2 mabatizo Neno hili hapa laweza kumaanisha ubatizo (kifupi “maziko” ndani ya maji) ya waamini katika Kristo, au laweza kumaanisha kuoga kimila tu kwa Kiyahudi.
  2. 6:1-2 kuwawekea watu mikono Tendo hilo lilikuwa ni njia ya kumwomba Mungu awabariki watu kwa njia maalumu kama vile kuwaponya, kumfanya Roho Mtakatifu aje ndani yao, au kuwapa nguvu kwa ajili ya kazi maalumu.
  3. 6:19 pazia Pazia la kiroho katika hekalu la kimbingu, lililoashiriwa na lile la kawaida lililotenganisha madhabahu ya ndani (na uwepo wa Mungu) kutoka katika chumba kingine ndani ya Hema Takatifu na katika Hekalu la Yerusalemu. Tazama Pazia katika Orodha ya Maneno. Pia katika 10:20.