Add parallel Print Page Options

Yesu Asema ni Lazima Afe

(Mk 8:31-9:1; Lk 9:22-27)

21 Kuanzia wakati huo Yesu alianza kuwaambia wafuasi wake kuwa ni lazima aende Yerusalemu. Alifafanua kuwa Viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria watamfanya apate mateso kwa mambo mengi. Na aliwaambia wafuasi wake kuwa lazima auawe. Na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.

22 Petro akamchukua Yesu na kwenda naye faragha mbali na wafuasi wengine. Akaanza kumkosoa Yesu kwa akasema, “Mungu akuepushe mbali na mateso hayo, Bwana! Hilo halitakutokea!”

23 Ndipo Yesu akamwambia Petro, “Ondoka kwangu, Shetani![a] Hunisaidii! Hujali mambo ya Mungu. Unajali mambo ambayo wanadamu wanadhani ni ya muhimu.”

24 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Ikiwa yeyote miongoni mwenu anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima aache kujiwazia yeye mwenyewe na mahitaji yake. Ni lazima awe radhi kuubeba msalaba aliopewa na kunifuata mimi. 25 Yeyote kati yenu anayetaka kuokoa uhai wake, ataupoteza. Lakini ninyi mlioyaacha maisha yenu kwa ajili yangu mtaupata uzima wa kweli. 26 Haina maana kwenu ninyi kuupata ulimwengu wote, ikiwa ninyi wenyewe mtapotea. Mtu atalipa nini ili kuyapata tena maisha yake baada ya kuyapoteza? 27 Mimi, Mwana wa Adamu, nitarudi katika utukufu wa Baba yangu pamoja na Malaika. Na nitamlipa kila mtu kutokana na matendo yake. 28 Niaminini ninaposema wapo watu waliopo hapa watakaoishi mpaka watakaponiona nikija kama Mwana wa Adamu kutawala kama mfalme.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 16:23 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Maana ya Yesu ni kuwa Petro alikuwa akiongea kama Shetani.