Petro Amponya Mlemavu Kwa Jina La Yesu

Siku moja Petro na Yohana walikwenda Hekaluni saa tisa kwa sala ya adhuhuri. Karibu na mlango uitwao Mzuri, palikuwa na mtu aliyekuwa amelemaa tangu kuzaliwa. Kila siku huyo mlemavu aliwekwa karibu na lango la Hekalu akawa akiomba fedha kwa watu waliokuwa wakiingia ndani ya Hekalu. Alipowaona Petro na Yohana wakielekea Hekaluni, aliwaomba wampe cho chote. Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tuangalie!” Akawakodolea macho akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

Lakini Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu za kukupa, lakini nitakupa kile nilicho nacho. Kwa jina la Yesu wa Nazareti nakuamuru, tembea!” Petro akamshika yule mtu mkono, akamwinua, akasimama kwa miguu yake mwenyewe. Mara miguu na viungo vyake vikapata nguvu. Akaruka juu, akasimama, akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akirukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walimwona akitembea na kumsifu Mungu 10 wakam tambua kuwa ni yule mlemavu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango akiomba omba. Wakashangaa mno kuhusu maajabu yaliyomtokea.

Petro Anashuhudia Kuwa Yesu Aponya

11 Yule mtu aliyeponywa alipokuwa bado anawang’ang’ania Petro na Yohana, watu wakawakimbilia mpaka kwenye ukumbi wa Sule mani wakiwa wamejawa na mshangao.

12 Petro alipoona watu wamekusanyika aliwaambia, “Watu wa Israeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao? Mnadhani ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemwezesha mtu huyu kutembea? 13 Sivyo! Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo na wa baba zetu amemtukuza mtumishi wake Yesu kwa muujiza huu. Ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato ijapokuwa Pilato alitaka kufuta mashtaka na kumwachilia. 14 Ninyi mlimkataa aliyekuwa Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule muuaji. 15 Hivyo mkamwua aliye chanzo cha Uzima, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa mambo haya. 16 Imani katika jina la Yesu imempa nguvu huyu mtu ambaye mnamwona na kumfahamu. Ni kwa jina la Yesu na imani inay opatikana kwake ambayo imemponya huyu mtu kabisa, kama ninyi wenyewe mnavyoona.

17 “Na sasa ndugu zangu, najua ya kuwa mambo mliyomtendea Yesu, ninyi na viongozi wenu, mliyafanya kwa kutokujua. 18 Lakini Mungu alikuwa ametabiri kwa njia ya manabii wake wote kwamba Kristo angeteswa, na hivi ndivyo alivyotimiza utabiri huo. 19 Kwa hiyo tubuni mumgeukie Mungu, ili azifute dhambi zenu, 20 na mpate nguvu za kiroho kutoka kwa Bwana. Naye atampeleka Kristo, yaani Yesu, ambaye alichaguliwa tangu awali kwa ajili yenu. 21 Yeye hana budi kukaa mbinguni mpaka wakati Mungu ataka pofanya kila kitu kuwa kipya tena, kama alivyotamka tangu zamani, kwa kupitia kwa manabii wake watakatifu. 22 Kama Musa alivy osema, ‘Bwana Mungu atawateulia nabii kati ya ndugu zenu kama alivyoniteua mimi. Mtamtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia. 23 Mtu ye yote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatengwa daima na watu wake na kuangamizwa.’

24 “Manabii wote tangu wakati wa Samweli na kuendelea pia walitabiri kuhusu siku hizi. 25 Ninyi ni wana wa manabii na wa ile ahadi ambayo Mungu aliwapa baba zenu, alipomwambia Abrahamu, ‘Kutokana na uzao wako familia zote ulimwenguni zitabarikiwa.’ 26 Mungu alipomfufua mtumishi wake alimtuma kwenu kwanza ili awaletee baraka kwa kuwawezesha kuacha uovu wenu.”