Petro Aeleza Alivyotumwa Kwa Mataifa

11 Baadaye mitume na waamini wa sehemu zote za Yudea wakapata habari kwamba watu wasiokuwa Wayahudi nao wamepokea neno la Mungu. Kwa hiyo Petro alipokwenda Yerusalemu, wale waliokuwa wakishikilia sheria ya tohara walimshutumu wakasema, “Kwa nini ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao?” Ndipo Petro akaanza kuwaeleza mambo yote yalivyotokea akasema, “Nil ikuwa nikiomba katika mji wa Jopa, nikaona katika ndoto kitu kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa ncha zake nne, kutoka mbinguni, nayo ikanifikia. Nilipotazama kwa makini nikaona wanyama wa kila aina, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. Nikasikia sauti ikiniambia, ‘Amka Petro, chinja, ule!’ Nami nikasema, ‘La, Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kili chokatazwa na sheria zetu.’ Lakini ile sauti kutoka mbinguni ikasema kwa mara ya pili, ‘Usiite kitu cho chote alichokitakasa Mungu kuwa ni uchafu.’ 10 Jambo hili lilitokea mara tatu ndipo vyote vikachukuliwa tena mpaka mbinguni. 11 Wakati huo huo watu watatu waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria wakawasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. 12 Roho akaniambia niende nao bila kusita. Nikaenda nao nikisindikizwa na hawa ndugu sita, tukaingia katika nyumba ya Kornelio. 13 Kornelio akatuambia jinsi malaika alivyomtokea akamwambia, ‘Tuma watu Jopa wakamwite Simoni aitwaye Petro. 14 Yeye anao ujumbe utakaokuokoa wewe na wote walio nyum bani mwako.’ 15 Nami nilipokuwa nikisema nao, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama alivyotushukia sisi mwanzoni. 16 Nami nikakumbuka jinsi Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.’ 17 Basi kwa kuwa Mungu ndiye aliyewapa hawa watu karama ile ile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu, mimi ni nani hata nimpinge Mungu?” 18 Nao waliposikia maneno haya hawakuwa na la kusema. Wakamsifu Mungu, wakasema, “Mungu amewapa watu wa mataifa nafasi ya kutubu na kupokea uzima wa milele.’ ’

Kanisa Laenea Antiokia

19 Wale waamini waliotawanyika kutoka Yerusalemu wakati wa mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, walisafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Wakawa wakihubiri Habari Njema kwa Wayahudi peke yake. 20 Lakini baadhi yao walikwenda Antiokia wakitokea Kipro na Kirene. Wakawaambia Wagiriki Habari Njema za Bwana Yesu. 21 Roho wa Bwana alikuwa pamoja nao kwa hiyo watu wengi wakaamini na kumgeukia Bwana. 22 Habari hizi zilipowafikia vion gozi wa kanisa huko Yerusalemu, walimtuma Barnaba aende Antiokia. 23 Alipofika akaona jinsi Mungu alivyokuwa akiwabariki watu kwa neema yake, alifurahi sana akawatia moyo waendelee kwa juhudi kuwa waaminifu kwa Bwana. 24 Barnaba alikuwa mtu mwema aliyejawa Roho Mtakatifu, mwenye imani kuu; na watu wengi waliongoka wakam wamini Bwana. 25 Kisha Barnaba akasafiri kwenda Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata akaja naye mpaka Antiokia. Na wote wawili wakakaa huko kwa mwaka mzima, wakiwafundisha wengi walioamini katika kanisa la Antiokia. Hapo Antiokia ndipo waamini waliitwa ‘Wakristo’ kwa mara ya kwanza.

27 Wakati huu manabii walitoka Yerusalemu wakaenda Antiokia. 28 Na mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama katika mkutano aka tabiri kwa uweza wa Roho kwamba pangetokea njaa kubwa dunia nzima. Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa mtawala. 29 Waamini wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada upelekwe kwa ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. 30 Wakafanya hivyo, na misaada ikapelekwa na Barnaba na Sauli kwa wazee wa kanisa.

Petro Arudi Yerusalemu

11 Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi[a] walimkosoa. Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”

Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”

“Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’

Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’

10 Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11 Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12 Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13 Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14 Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’

15 Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.[b] 16 Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”

18 Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”

Habari Njema Zafika Antiokia

19 Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso[c] yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20 Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.[d] Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21 Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.

22 Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.

25 Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.[e]

27 Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28 Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29 Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote[f] wanaoishi Uyahudi. 30 Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.

Footnotes

  1. 11:2 waamini wa Kiyahudi Kwa maana ya kawaida, “watu wa tohara”. Hii inaweza kuwa na maana ya Wayahudi waliodhani kuwa wafuasi wote wa Kristo ni lazima watahiriwe na kutii Sheria ya Musa. Tazama Gal 2:12.
  2. 11:15 mwanzo Siku ya Pentekoste katika Matendo 2, Roho Mtakatifu alipowashukia wafuasi wa mwanzo wa Yesu na kuwapa nguvu ya kuanza kuuhubiri ulimwengu Habari Njema za wokovu kupitia Yesu.
  3. 11:19 mateso Au “kipindi cha mateso”. Hiki ni kipindi ambacho viongozi wa Kiyahudi katika mji wa Yerusalemu walikuwa wakiwaadhibu watu wanaomwamini Kristo. Tazama Mdo 8:1-4.
  4. 11:20 watu wasio Wayahudi Kwa maana ya kawaida, “Wa mataifa” au “Wahelenisti”, au watu waliochangamana na kuathiriwa na utamaduni wa Kiyunani (Kigiriki). Nakala zingine za Kiyunani zina “Wayunani” au “Wagiriki”.
  5. 11:26 Wafuasi wa Kristo Yaani, Wakristo.
  6. 11:29 ndugu wote Yaani, Jamaa yote ya Waamini.