Add parallel Print Page Options

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mt 9:1-8; Lk 5:17-26)

Siku chache baadaye Yesu alirudi Kapernaumu na habari zikaenea kuwa yupo nyumbani. Hivyo watu wengi walikusanyika kumsikiliza akifundisha na haikuwapo nafasi iliyobaki kabisa ndani ya nyumba, hata nje ya mlango. Yesu alipokuwa akifundisha, baadhi ya watu walimleta kwake mtu aliyepooza amwone. Mtu huyo alikuwa amebebwa na rafiki wanne. Watu hao hawakuweza kumfikisha mgonjwa kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu ulioijaza nyumba yote. Hivyo walipanda na kuondoa paa juu ya sehemu aliposimama Yesu. Baada ya kutoboa tundu darini[a] kwenye paa, wakateremsha kirago alimokuwa amelala yule aliyepooza. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo wale waliomleta na yule mwenye kupooza, alimwambia, “Mtoto wangu, dhambi zako zimesamehewa.”

Baadhi ya walimu wa sheria walikuwa wamekaa pale. Nao waliona kile alichokifanya Yesu na wakawaza miongoni mwa wenyewe, “Kwa nini mtu huyu anasema maneno kama hayo? Si anamtukana Mungu! Kwani hakuna awezaye kusamehe dhambi ila Mungu.”

Mara moja Yesu alifahamu walichokuwa wakikifikiri wale walimu wa sheria, hivyo akawaambia, “Kwa nini mna maswali kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kirago chako na utembee’? 10 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina!” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? 11 Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kirago chako uende nyumbani!’”

12 Yule mtu aliyepooza alisimama na bila kusita, akabeba kirago chake na akatoka nje ya nyumba wakati kila mmoja akiona. Matokeo yake ni kuwa wote walishangazwa na mambo hayo. Wakamsifu Mungu na kusema, “Hatujawahi kuona kitu kama hiki!”

Read full chapter

Footnotes

  1. 2:4 kutoboa tundu darini Au “wametoboa tundu darini”.