Add parallel Print Page Options

Yesu Amponya Mgonjwa

(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)

40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”

41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[a] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.

43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[b] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[c] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.

Read full chapter

Footnotes

  1. 1:41 akakasirika Nakala nyingi za Kiyunani zimetumia “Akajawa na huruma …”. Lakini ni vigumu kuelezea kwa nini tafsiri za Kiyunani na zile za Kilatini zimekuwa na “Akijawa na hasira …”, Kwa hiyo wasomi wengi zama za leo hudhani hivyo ndivyo ilivyosomeka awali.
  2. 1:44 akakuchunguze Ama akakukague. Sheria ya Musa iliagiza kwamba kuhani anapaswa kuthibitisha kama mwenye ukoma sasa amepona.
  3. 1:44 aliamuru Yaani alizoagiza Musa tazama Law 14:1-32.