Mitume Wa Kristo

Basi, mtuhesabu sisi kuwa watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu. Zaidi ya hayo, mawakili wanatakiwa wawe waaminifu. Mimi sijali kama ninyi mkinihukumu au nikihukumiwa na mahakama ya wanadamu; kwa kweli hata mimi mwenyewe sijihukumu Dhamiri yangu hainishitaki; lakini hilo halinifanyi nisiwe na hatia. Bwana ndiye anayenihukumu. Kwa hiyo msitoe hukumu kabla ya wakati wake, kabla Bwana hajaja. Yeye atafichua mambo yaliyof ichwa gizani na kwa kuweka wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mtu atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

Basi ndugu zangu nimetumia mfano wa Apolo na mimi kwa faida yenu ili muweze kujifunza kutoka kwetu maana ya usemi, “Usivuke mpaka wa yale yaliyoandikwa.” Na hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. Ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na watu wengine wote? Mna kitu gani ambacho hamkupokea? Basi ikiwa mmepokea, mbona mnajivuna kana kwamba hayo mliyonayo si zawadi?

Mmekwisha pata kila kitu mnachohitaji! Mmekuwa matajiri! Mmekuwa wafalme pasipo msaada wetu! Lakini laiti kama mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tuwe wafalme pamoja nanyi! Kwa sababu inaonekana kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa katika msafara wa maonyesho kama watu waliohukumiwa kufa hadharani, kwa sababu tumekuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia.

10 Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima ndani ya Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. 11 Mpaka wakati huu tuna njaa na kiu, tumevaa matambara, tumeteswa, hatuna makao. 12 Tunafanya kazi ngumu kwa mikono yetu. Tunapolaaniwa, tunabar iki; tunapoteswa tunavumilia. 13 Tunaposingiziwa tunajibu kwa maneno ya upole. Tumekuwa kama takataka ya dunia hii, na uchafu wa ulimwengu mpaka leo hii.

14 Nawaandikia mambo haya, si kwa sababu nataka muone aibu, bali nataka niwaonye kama wanangu wapendwa. 15 Ingawa mnao viongozi wasiohesabika katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Kristo Yesu kwa kuwaletea Injili. 16 Basi nawasihi mfuate mfano wangu. 17 Kwa sababu hii ninam tuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu maisha yangu katika Kristo ambayo yanakubal iana na mafundisho yangu katika kila kanisa ninalotembelea.

18 Baadhi yenu mmekuwa na kiburi mkidhani kuwa sitafika kwenu. 19 Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, zaidi ya maneno yao hawa watu wenye kiburi wana uwezo gani? 20 Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu bali ni nguvu. 21 Ninyi amueni. Nije kwenu na fimbo kuwaadhibu, au nije na upendo kwa roho ya upole?

Mitume wa Kristo Yesu

Tuchukulieni sisi kuwa ni watumishi wa Kristo, ambao Mungu ametuamini tufanye kazi ya kuwaambia wengine siri zake za kweli. Wale walioaminiwa kwa kazi muhimu kama hii imewapasa kuonesha ya kuwa wao ni waaminifu. Lakini siichukulii hukumu yenu kuhusu hili kuwa kitu. Hata hukumu yo yote katika mahakama ya kibinadamu isingekuwa na maana yoyote. Sijihukumu hata mimi mwenyewe. Sikumbuki kosa lolote nililofanya, lakini hiyo hainifanyi mimi kujihesabia haki. Bwana pekee ndiye anayepaswa kunihukumu ikiwa nimefanya vyema au la. Hivyo, msimhukumu mtu yeyote sasa. Hukumu itakuwa wakati Bwana atakaporudi. Ataangaza mwanga kwa kila kitu kilichofichwa gizani. Ataziweka wazi nia za siri za mioyo yetu. Ndipo sifa ambayo kila mtu anapaswa kuipata itatoka kwa Mungu.

Ndugu zangu, nimemtumia Apolo na mimi mwenyewe kama mfano kwa ajili yenu. Nimefanya hivi ili mjifunze kutoka kwetu maana ya maneno yanayosema, “Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa.”[a] Kwa nini mnajisifu? Mlipewa kila kitu mlicho nacho. Sasa, ikiwa mlipewa kila kitu mlicho nacho, kwa nini mnajisifu kana kwamba mlipata vitu vyote kwa nguvu zenu wenyewe?

Mnadhani kwamba tayari mna kila kitu mnachohitaji. Mnadhani kwamba mmekwisha tajirika. Laiti mngekwisha fanywa wafalme, kwa sababu tungekuwa wafalme pamoja nanyi. Lakini inaonekana kana kwamba Mungu amenipa mimi na mitume wengine mahali pa mwisho. Sisi ni kama wafungwa waliohukumiwa kufa, waliosimamishwa katika gwaride ili ulimwengu wote uwaone, si watu tu bali hata malaika pia. 10 Tu wapumbavu kwa kuwa sisi ni wa Kristo, lakini mnadhani kuwa ninyi ni wenye hekima katika Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini mnadhani kuwa mna nguvu. Watu wanawaheshimu ninyi, na hawatuheshimu sisi. 11 Hata sasa hatuna vyakula vya kutosha kula au kunywa, na hatuna nguo za kutosha. Mara kwa mara tunapigwa na hatuna makazi. 12 Tunafanya kazi sana kwa mikono yetu ili tupate chakula. Watu wanapotutukana, tunamwomba Mungu awabariki. Watu wanapotutendea vibaya, tunavumilia. 13 Watu wanaposema mabaya juu yetu, tunawajibu kwa upole. Lakini watu wanaendelea kutuona kama takataka.

14 Siwaambii haya ili kuwatahayarisha, lakini ninaandika haya ili kuwaonya kama watoto wangu mwenyewe ninaowapenda. 15 Mnaweza kuwa na walimu elfu kumi katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Kupitia Habari Njema mimi nilifanyika baba kwenu katika Kristo Yesu. 16 Ndiyo sababu ninawahimiza mfuate mfano wangu. 17 Ndiyo sababu ninamtuma Timotheo kwenu. Ni mwanangu katika Bwana. Ninampenda na ni mwaminifu. Atawasaidia ili mkumbuke namna ninavyoishi kama mfuasi wa Kristo Yesu, kama ninavyofundisha katika kila kanisa kila mahali ninakokuwa.

18 Baadhi yenu mnajivuna, mkidhani kuwa sitakuja kuwatembelea tena. 19 Lakini nitakuja kwenu hivi karibuni ikiwa Bwana atanijalia. Ndipo nitajua ikiwa hawa wanaojivuna wana nguvu za kutenda jambo lolote zaidi ya kuzungumza. 20 Mungu huonesha kuwa anatawala katika maisha kwa yale wanayoweza kufanya na si kwa maneno yao. 21 Je, nitakapokuja kwenu, nije nikiwa na adhabu au nije kwa upendo na upole?

Footnotes

  1. 4:6 Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa Kwa maana ya kawaida, “Msifanye zaidi ya kile kilichoandikwa”. Hii ina maana ya Maandiko ama usemi maarufu, mfumo ama kanuni kwamba walimu walitumia watoto kuandika alfabeti. Paulo anawatia moyo Wakorintho wafuate mfano huo.